[theme_section_hidden_section.ReportAbuse1] : Plus UI currently doesn't support ReportAbuse gadget added from Layout. Consider reporting about this message to the admin of this blog. Looks like you are the admin of this blog, remove this widget from Layout to hide this message.
Kwa nini Wazee Huathirika Zaidi?
Wataalamu wa afya wanabainisha kuwa kadri umri unavyoongezeka, viungo vya mwili kama moyo, figo, mapafu, na mifumo mingine ya mwili huanza kuchakaa kutokana na matumizi ya muda mrefu. Hali hii huambatana na mtindo wa maisha usiofaa, ikiwa ni pamoja na ulaji wa vyakula visivyofaa, kutofanya mazoezi, matumizi ya tumbaku na pombe, na kutokuwa na mpangilio mzuri wa maisha ya kila siku.
Magonjwa Hatari kwa Wazee
Magonjwa yanayowaathiri wazee zaidi ni pamoja na:
Shinikizo la juu la damu
Kisukari
Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu
Kiharusi (stroke)
Unene uliopitiliza
Lehemu (cholesterol) nyingi
Saratani mbalimbali
Magonjwa ya figo sugu
Matatizo ya mfumo wa upumuaji
Magonjwa ya akili kama sonona na kupoteza kumbukumbu (dementia)
Aidha, matatizo ya mifupa, viungo na kusinyaa kwa misuli ni changamoto nyingine zinazowakumba wazee, na kusababisha utegemezi mkubwa kwa wengine.
Namna ya Kujikinga: Hatua Muhimu kwa Wazee
Ili kupunguza athari za magonjwa haya, wazee wanapaswa kuchukua hatua za makusudi, zifuatazo:
Lishe Bora
Kula mbogamboga na matunda kwa wingi
Kuweka kipaumbele kwa protini za mimea (kama karanga, maharagwe, dengu)
Kupunguza ulaji wa chumvi, sukari, wanga na mafuta mengi
Kuepuka vyakula vya kukaanga au vyenye mafuta mengi
Mazoezi na Shughuli za Mwili
Kutembea kwa angalau dakika 30 kwa siku, siku 5 kwa wiki
Kufanya kazi nyepesi za nyumbani kama usafi na bustani
Mazoezi mepesi ya viungo kwa wale wasio na uwezo mkubwa wa kutembea
Kulala na Kupumzika
Kupata usingizi wa saa 7–8 kwa usiku mmoja
Kupata burudani ya kiakili kama kusikiliza muziki, kusoma au kushiriki mijadala yenye manufaa
Kupunguza msongo wa mawazo na kujitenga na hali za mfadhaiko
Uchunguzi wa Afya wa Mara kwa Mara
Kufanya uchunguzi wa afya wa jumla kila baada ya miezi sita
Kujua viwango vya sukari, shinikizo la damu, lehemu, na afya ya figo na ini mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa
Kumtembelea mtaalamu wa lishe kwa mwongozo wa chakula bora
Kuishi katika Mazingira Bora
Kuepuka maeneo yenye kelele au uchafuzi wa hewa
Kuishi kwenye maeneo salama, yenye mwanga wa kutosha na ubaridi wa kawaida
Hitimisho
Umri wa uzee ni kipindi cha hekima na utulivu, lakini pia huambatana na changamoto nyingi za kiafya. Hata hivyo, kwa mitindo bora ya maisha, lishe nzuri, mazoezi na uchunguzi wa afya wa mara kwa mara, wazee wanaweza kuishi maisha marefu yenye afya bora, furaha na heshima. Serikali, familia na jamii kwa ujumla zinapaswa kushirikiana kuwahudumia wazee kwa upendo, ili waweze kuendelea kuwa nguzo muhimu ya maarifa, maadili na mshikamano katika jamii.